19/09/2025
BREAKING : Shirika la Afya Duniani (WHO) limethibitisha kuwa wagonjwa 31 kati ya 38 waliothibitishwa kuambukizwa virusi vya Ebola wamefariki dunia katika eneo la kusini mwa Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo, ambako mamlaka zinaendelea kukabiliana na mlipuko mpya wa ugonjwa huo hatari.
Takwimu za hivi karibuni zinaonyesha kuwa kiwango cha vifo kimeongezeka mara mbili ikilinganishwa na wiki iliyopita, kutoka vifo 16, huku ugonjwa huo ukiendelea kusambaa kwa kasi. Kwa mujibu wa WHO, zaidi ya watu 900 waliowahi kuwa karibu na wagonjwa wamebainishwa. Hatua za utoaji wa chanjo zilianza Jumapili katika maeneo yaliyoathirika, ambapo wahudumu wa afya zaidi ya 500 pamoja na watu waliokuwa karibu na wagonjwa tayari wamepokea chanjo hiyo, jambo linalowapa kinga muhimu, amesema Dkt. Patrick Otim kutoka programu ya WHO Afrika.
Mamlaka za Congo zilitangaza rasmi mlipuko mpya wa Ebola mnamo Septemba 5 katika eneo la Bulape, mkoa wa Kasai, ulioko katikati mwa nchi karibu na mpaka wa Angola.
Wiki iliyopita, Kituo cha Afrika cha Kudhibiti na Kuzuia Magonjwa (Africa CDC) kiliripoti kuwa ugonjwa huo umeenea kutoka wilaya mbili hadi nne.
Kwa mujibu wa Sheillah Nsasiirwe, Afisa wa Dharura za Afya na Chanjo katika WHO Afrika, shehena mpya ya chanjo iliyoidhinishwa na Kundi la Kimataifa la Kuratibu Upatikanaji wa Chanjo (ICG) inatarajiwa kuwasili kuanzia Ijumaa hadi Jumapili.
“Utekelezaji wa chanjo haujakamilika kwa kasi tuliyokusudia kutokana na changamoto za upatikanaji na ucheleweshaji wa usafirishaji wa chanjo,” alisema. Maafisa wa WHO wameeleza kuwa chanjo hizo zimesafirishwa kwa mafungu madogo kwa sababu ya ukosefu wa miundombinu ya kuhifadhia chanjo katika eneo la Bulape.