26/08/2026
Mshambuliaji wa Simba SC, Ibrahim Doumbia, amekuwa gumzo miongoni mwa mashabiki wa klabu hiyo, huku mjadala mkubwa ukiendelea kuhusu uwezo wake na k**a anaendana na mfumo wa timu.
Baadhi ya mashabiki wameanza kukosoa kasi na namna anavyocheza, wakiona bado hajawa kwenye kiwango kinachotarajiwa.
Lakini upande mwingine unaamini Doumbia anahitaji muda na uvumilivu ili kuzoea ligi na mazingira mapya.
Mjadala huo umechochewa zaidi na mechi za hivi karibuni, ambapo mshambuliaji huyo amekuwa akionekana kupata ugumu kuendana na kasi ya mchezo wa Simba kila anapopewa nafasi.
Hata hivyo, taarifa kutoka ndani ya benchi la ufundi zinaeleza kuwa Kocha Mkuu Steve Barker amefanya mazungumzo ya faragha na Doumbia, akimtaka kuongeza juhudi katika maeneo yenye mapungufu huku akiendelea kumpa nafasi taratibu.
Barker anaamini kadiri Doumbia atakavyopata muda zaidi uwanjani, ndivyo atakavyozidi kuzoea mfumo wa Simba na kurejesha makali yake ya kufunga.
Kabla ya kujiunga na Simba, Doumbia alikuwa mfungaji bora wa Ligi Kuu ya Mali msimu uliopita akiwa na AS Korofina. Huko, mfumo wa timu ulimruhusu kucheza zaidi ndani ya boksi, huku mawinga wakitengeneza nafasi kwa kupiga krosi.
Lakini Simba inacheza kwa mtindo tofauti. Mawinga mara nyingi hukata kuelekea ndani, huku timu ikisisitiza zaidi mpira wa chini na kutengeneza nafasi katika maeneo finyu, badala ya kutegemea krosi mara kwa mara.
Tofauti hiyo ya mifumo inaonekana kuwa moja ya changamoto zinazomkabili Doumbia, ambaye sasa anatakiwa pia kushuka chini, kushiriki ujenzi wa mashambulizi na kutengeneza nafasi badala ya kusubiri mipira ndani ya boksi.
Katika michezo ya hivi karibuni, Barker amekuwa akimtumia Elie Mpanzu k**a mshambuliaji kivuli, huku Doumbia akiingia zaidi kipindi cha pili.
Swali linalobaki ni moja: Doumbia bado anahitaji muda tu, au mfumo wa Simba ndio unaomfanya ashindwe kuonyesha makali yake?