09/02/2021
NUNDA MZEE
NA MARTIN MAZUGWA
Kitu kilichowastaajabisha si kwasababu vilikataliwa na kila mtu la hasha bali ni jinsi vilivyokuwa vimefungwa kwa ustadi mkubwa na mmiliki wake ambaye hadi wakati huo alikuwa hajajulikana.
Kilichowashtua wengi ni jinsi viroba hivyo vivyokuwa na muonekano k**a maiti iliyoviringishwa ndani ya sanda na tayari kwa kuzikwa.
Jambo hilo liliwagutusha wavuvi hao ambao baadhi wakakata shauri na kutaka kuvifungua viroba hivyo kujionea kilichomo ndani, lakini Mzee Masanja Bundala, ambaye ni mkongwe katika kazi ya uvuvi akawaonya vijana hao ambao tayari walianza kutafuta kisu ilikukata kamba.
Mzee Bundala ambaye ni mzaliwa wa Shinyanga, katika Wilaya ya Kahama ambaye aliondoka huko kuukimbia ukata alikuja jijini Dar es Salaam, kutafuta maisha kutokana na magumu aliyokutana nayo huko alikotoka.
Baada ya kutafuta kazi katika viwanda na taasisi mbalimbali za kiserikali na zile za watu binafsi bila mafanikio ndipo akaangukia katika kazi ya uvuvi ambayo alianza kuifanya tangu miaka ya 1980.
Kwa miaka yote hiyo mzee alikuwa mtu wa kutwa kucha baharini akisaka samaki kwaajili ya kitoweo cha yeye na familia yake ambayo ilikuwa na watoto wawili wa k**e na kiume ambao alibaki nao baada ya mkewe kufariki.
Hivyo aliijua vyema bahari na tabia zake kutokana na kupitia maswahibu mengi ndio maana aliwaonya vijana kuacha haraka kukurupukia jambo ambalo wamepata kuliona kwa mara ya kwanza.
Baada ya kuwasihi kuacha papara katika jambo geni vijana hao wanaamua kutulia na kufuata busara za mzee huyo ambaye alikuwa akiheshimika sana kutokana na busara zake.
***
IKIWA ndio kwanza asubuhi purukushani zilikuwa zikiendelea katika kituo kidogo cha Polisi cha Kawe kilichopo Ukwamani, askari waliokuwa wakiingia kazini wengine walianza kutoka baada ya kumaliza lindo la usiku.