05/06/2026
MBWA ALIYENGOJA MPAKA MWISHO
Mwaka 1924 nchini Japan, profesa mmoja aitwaye Hidesaburō Ueno alimchukua mbwa mdogo wa aina ya Akita na kumpa jina la Hachikō.
Kila asubuhi, Hachikō alikuwa akimsindikiza mmiliki wake hadi kituo cha treni cha Shibuya Station. Jioni, alikuwa akirudi kituoni hapo kumsubiri profesa wake arudi kutoka kazini.
Hili lilikuwa jambo la kawaida kila siku.
Lakini siku moja, profesa alipata tatizo kubwa la afya akiwa kazini na akafariki dunia ghafla. Hakuwahi kurudi tena kituoni.
Hachikō hakujua kilichotokea.
Jioni ile alienda kituoni na kusubiri.
Siku iliyofuata alirudi tena.
Kisha siku nyingine.
Wiki zikawa miezi, na miezi ikawa miaka.
Kwa karibu miaka 10, Hachikō aliendelea kwenda kituoni kila siku kumsubiri mmiliki wake aliyempenda sana. Hakujali mvua, jua wala baridi. Aliamini siku moja angerudi.
Watu waliokuwa wakipita kituoni waliguswa sana na uaminifu wake. Walianza kumpatia chakula na kumtunza. Habari zake zikaenea kote nchini Japan.
Alipofariki mwaka 1935, watu wengi walihuzunika. Hadi leo kuna sanamu yake nje ya kituo cha Shibuya k**a kumbukumbu ya uaminifu wake wa ajabu.
Funzo la Maisha: Uaminifu wa kweli huonekana zaidi wakati hakuna faida ya kuupata.
Swali: Je, ungekuwa mmoja wa watu waliomwona Hachikō akingoja kila siku, ungefanya nini kumsaidia? ❤️🐕