11/08/2026
🇺🇸 TRUMP AFICHWA KWENYE LORI ABADILISHA NDEGE KWA SIRI BAADA YA TISHIO LA IRAN
Vyombo vya habari nchini Marekani vimeripoti kuwa Rais wa Marekani, Donald Trump, alihamishwa kwa siri kutoka kwenye ndege ya Air Force One wakati akiondoka kwenye mkutano wa kilele wa NATO nchini Uturuki mwezi uliopita, kutokana na tishio linalodaiwa kutoka Iran.
Kwa mujibu wa gazeti la The Washington Post, Trump alionekana mbele ya kamera akipanda Air Force One, lakini baadaye alihamishwa kwa siri kupitia gari la huduma ya chakula la uwanja wa ndege, ambalo lilimpeleka hadi kwenye ndege ndogo ya kijeshi aina ya C-32A.
Operesheni hiyo inadaiwa kufanyika bila baadhi ya wafanyakazi wa Ikulu pamoja na waandishi wa habari waliokuwa kwenye ndege ya awali kujua kwamba Trump tayari alikuwa amehamishiwa kwenye ndege nyingine.
Maafisa wa Marekani waliambia CBS News kuwa kulikuwa na tishio linaloaminika kutoka Iran dhidi ya Trump, jambo lililosababisha hatua hiyo ya kiusalama.
Awali, Trump alikuwa amesema kuwa yeye ndiye “lengo namba moja” la Iran wakati wa ziara yake nchini Uturuki.
Ikulu ya Marekani bado haijathibitisha rasmi taarifa kuhusu mpango huo wa siri wa kubadilisha ndege.