25/05/2026
Simba wameingia rasmi kwenye mbio za kuwania saini ya mshambuliaji hatari wa ASEC Mimosas, Kelvin Bakare, raia wa Ivory Coast ambaye amekuwa kwenye kiwango bora msimu huu.
Taarifa zinaeleza kuwa uongozi wa Simba umeanza kufanya mawasiliano ya awali kwa ajili ya kumfuatilia mshambuliaji huyo wenye kasi, nguvu na umaliziaji mzuri ndani ya ligi ya Ivory Coast. Bakare ameonyesha kiwango cha juu akiwa na ASEC Mimosas, ambapo ameripotiwa kufunga mabao 17 katika mashindano mbalimbali msimu huu na kuwa sehemu muhimu ya mafanikio ya klabu hiyo kutwaa ubingwa.
Mshambuliaji huyo ameendelea kuvutia macho ya vilabu kadhaa kutokana na uwezo wake mkubwa wa kucheza k**a namba 9 wa kisasa, huku akitajwa kuwa na uwezo mkubwa wa kushambulia mipira ya juu, kucheza kwa nguvu pamoja na kutengeneza nafasi ndani ya eneo la hatari. Kiwango chake hicho kimeifanya Simba kuona kuwa anaweza kuwa suluhisho la kuongeza makali ya safu yao ya ushambuliaji kuelekea msimu mpya wa mashindano ya ndani na kimataifa.
Hata hivyo, Simba haitakuwa peke yake katika mbio hizo kwani taarifa zinaeleza kuwa klabu ya Al Masry kutoka Misri pamoja na Grenoble Foot inayoshiriki Ligue 2 nchini Ufaransa nazo zimeonyesha nia ya kuhitaji huduma za mshambuliaji huyo. Ushindani huo unaweza kufanya dili hilo kuwa gumu kutokana na thamani yake kuendelea kupanda baada ya msimu mzuri aliokuwa nao akiwa na Asec mimosas.